Kwa miaka kadhaa sasa, Kigamboni Awards imekuwa ikitajwa kama moja ya majukwaa yanayochipua kwa kasi kwenye tasnia ya filamu Tanzania.
Kilichoanza kama jukwaa la kutoa nafasi kwa wasanii wa Kigamboni, sasa kinaonekana kuanza kujenga sura mpya ya ushindani wa filamu nje ya mipaka ya wilaya hiyo.
Ndani ya mahojiano maalum na Sauti za Filamu, Mike Nondo ambaye ni Katibu wa Chama cha Waigizaji Wilaya ya Kigamboni pamoja na Katibu na Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, amesema msimu wa nne wa mwaka 2026 unakuja na mabadiliko makubwa ambayo yataibadilisha kabisa taswira ya Kigamboni Awards.
“Tulipoanza mwaka 2023 tulikuwa tunaangalia zaidi Kigamboni na maeneo ya karibu ndani ya Dar es Salaam. Lakini sasa tunazungumza kuhusu mikoa mitano. Tunayo Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Tanga pamoja na Zanzibar,” amesema Mike.
Mike anaeleza kuwa ndoto yao si kufanya event ya kawaida ya kila mwaka, bali kujenga tamasha litakalokuwa kivutio cha kitaifa kwa watengeneza filamu kutoka kila kona ya Tanzania.
“Tunataka ifike hatua mtu anatoka Kigoma, Bukoba au Tabora anafunga safari kuja Kigamboni kushindana. Kama ilivyo kwenye matamasha makubwa mengine, watu wajue kuna kipindi fulani lazima waende Kigamboni kwa ajili ya filamu.”
Katika mahojiano hayo, Mike ameweka wazi kuwa siri kubwa ya ukuaji wa tamasha hilo imekuwa ni kutorudia mfumo uleule kila mwaka.
Waandaaji wamekuwa wakifanya maboresho ya mara kwa mara kwenye ubora wa tuzo maandalizi ya siku ya tukio, pamoja na thamani ya ushindi wenyewe.
Anasema tofauti kati ya msimu wa kwanza na wa sasa ni kubwa kiasi kwamba washiriki wenyewe wanaanza kuona thamani yake.
“Kila mwaka lazima kuwe na utofauti. Ukifanya kitu kilekile watu wanachoka. Ndiyo maana tulibadilisha ubora wa tuzo yenyewe, tukaboresha ukumbi na kuanzia msimu wa tatu washindi wakaanza kupata fedha taslimu pamoja na tuzo,” amesema.
Sasa Kigamboni Awards imeanza kuweka fedha mezani kwa washindi wake jambo linalopambaniwa kwa imani kubwa sana na Mike, na uongozi wa Kigamboni Awards.
Mpaka sasa, zikiwa zimebaki siku chache kabla dirisha la ushiriki kufungwa rasmi, tayari zaidi ya filamu 300 zimewasilishwa kupitia mfumo wa kuwasilisha mitandaoni.
Idadi hiyo ni kubwa sana kuwahi kushuhudiwa tangu tamasha hilo lianzishwe.
“Mwaka huu mwitikio ni mkubwa sana. Watu wana-submit kazi kutoka maeneo mbalimbali. Hii inaonyesha Kigamboni Awards inaanza kuaminika zaidi kwenye tasnia, nchini.”
Mbali na ushindani wa filamu, Mike amesema waandaaji pia wameimarisha mifumo ya kura pamoja na majaji ili kuhakikisha uwazi na haki vinatawala kwenye matokeo ya mwisho.
Kuna uwezekano mkubwa wa hafla hiyo kufanyika katika ukumbi wa hukohuko Kigamboni ili kutoa faragha kwa viongozi pamoja na wageni mashuhuri wanaotarajiwa kuhudhuria.
Hata hivyo, pamoja na hatua hizo zote, Mike hakuficha changamoto zinazoendelea kuikabili tasnia ya matamasha ya filamu nchini.
Udhamini wa kifedha pamoja na mwitikio mdogo wa baadhi ya vyombo vya habari kwenye habari za sanaa zenye kujenga tasnia vimekuwa ni tatizo linalokua.
Lakini pamoja na changamoto hizo haizuii hata chembe kukua kwa Kigamboni Awards na kwa mwendo huu, huenda Kigamboni ikawa moja ya vituo vikubwa vya ushindani wa filamu Tanzania katika miaka michache ijayo.