Na Charles Mkoka
Kwa miaka mingi, filamu zimekuwa zikitazamwa kama sehemu ya burudani. Lakini kadri changamoto za kijamii zinavyozidi kuongezeka, nafasi ya filamu katika kuelimisha na kuhamasisha mabadiliko imeendelea kupata uzito mpya.
Hilo limejitokeza tena kupitia uzinduzi wa filamu ya Kifurushi, kazi maalum iliyotayarishwa kwa lengo la kutoa elimu kuhusu athari za usafirishaji wa dawa za kulevya na umuhimu wa kufuata taratibu sahihi wakati wa kusafirisha mizigo.
Filamu hiyo ilizinduliwa Juni 12, 2026 katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam, katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali, wadau wa sekta ya usafirishaji pamoja na wasanii na wanatasnia wa filamu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, alisema matumizi ya filamu katika kampeni za kijamii yanaonesha nguvu kubwa ambayo sanaa hiyo imekuwa nayo katika kufikisha ujumbe kwa wananchi.
“Filamu ni nyenzo yenye nguvu katika kuelimisha na kuleta mabadiliko chanya ya tabia katika jamii,” alisema Dkt. Kasiga.
Kwa mujibu wake, uwezo wa filamu kusimulia maisha halisi na kuwagusa watazamaji kihisia unaifanya kuwa njia yenye ufanisi mkubwa wa kufikisha ujumbe kuliko mbinu nyingi za mawasiliano zinazotumika katika kampeni za kijamii.
Filamu Kifurushi imeandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa uratibu wa Bodi ya Filamu Tanzania. Kazi hiyo inaelezea namna watu wanavyoweza kujikuta wakihusishwa na makosa ya dawa za kulevya kwa kubeba mizigo au vifurushi wasivyovifahamu.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas James Lyimo, aliyehudhuria kama mgeni rasmi, alisema filamu hiyo itaanza kuoneshwa katika mabasi yaendayo mikoani ili kuwafikia maelfu ya wananchi wanaosafiri kila siku.
Hatua hiyo inaonesha mwelekeo mpya wa matumizi ya filamu nchini, ambapo kazi za kisanaa zinaanza kutumika moja kwa moja katika kampeni za kitaifa zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.
Dkt. Kasiga aliwataka wadau wa sekta za umma na binafsi kuona filamu kama mshirika muhimu wa maendeleo, akisisitiza kuwa milango ya Bodi ya Filamu Tanzania iko wazi kwa taasisi zinazotaka kutumia sanaa kufikisha ujumbe kwa jamii.
Uzinduzi wa Kifurushi umeenda sambamba na kaulimbiu ya “Usafiri Salama Bila Dawa za Kulevya,” huku ukiacha ujumbe mmoja muhimu kwa wadau wa tasnia: filamu inaweza kuwa zaidi ya burudani. Inaweza kuwa darasa, kampeni na sauti ya mabadiliko ndani ya jamii.