Tanzania yamuaga gwiji wa maigizo Mzee Onyango, viongozi na wasanii wamuenzi

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Tanzania imemuaga  mmoja wa magwiji wa sanaa ya maigizo, Issa Joseph Mohamed maarufu kama Mzee Onyango, aliyepumzishwa katika Makaburi ya Kondo, Ununio, baada ya mamia ya watu kujitokeza kutoa heshima za mwisho kwa msanii huyo aliyegusa maisha ya wengi kupitia kazi zake.

Katika shughuli ya kuaga mwili wake iliyofanyika nyumbani kwake Kawe jijini Dar es Salaam, viongozi wa serikali, wasanii, ndugu, jamaa na mashabiki walikusanyika kumuenzi msanii huyo ambaye kwa miongo kadhaa alikuwa sehemu ya historia ya maigizo ya Tanzania.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria shughuli hiyo alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, aliyeambatana na mkewe, Mariam Mwinyi.

Ingawa hakutoa salamu hadharani, uwepo wa Rais Mwinyi uliashiria heshima kubwa ambayo Mzee Onyango alikuwa nayo katika jamii na mchango wake katika sekta ya sanaa nchini.

Akizungumza wakati wa kuaga mwili wa marehemu, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema Tanzania imepoteza mmoja wa wasanii walioweka msingi imara wa tasnia ya maigizo.

“Mzee Onyango alikuwa mpendwa wa watu wengi. Leo tunaona umati mkubwa wa waombolezaji uliokusanyika hapa kwa sababu aligusa maisha ya watu wengi kupitia kazi zake za sanaa,” amesema.

Mwinjuma amesema marehemu alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa maigizo yaliyovuka kutoka enzi za redio kwenda kwenye televisheni.

Licha ya wengi kumhusisha na mataifa jirani kutokana na lafudhi yake na namna alivyocheza baadhi ya nafasi zake, Mzee Onyango alikuwa Mtanzania halisi mwenye ucheshi wa asili uliobaki kuwa sehemu ya utambulisho wake hadi siku zake za mwisho.

Devotha Helman amewashukuru Watanzania wote waliokuwa pamoja na marehemu wakati wa ugonjwa wake pamoja na wale waliojitokeza kushiriki msiba.

Amesema familia imefarijika kuona upendo mkubwa ulioonyeshwa na wananchi, viongozi, wasanii na wataalamu wa afya wa Hospitali ya Jeshi ya Lugalo waliomhudumia marehemu katika siku zake za mwisho.

“Kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa katika familia yetu na kwa Watanzania wengi waliomfahamu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi mzee wetu Onyango,” amesema.


Kwa upande wa wasanii, wengi wameeleza kuwa kifo cha Mzee Onyango ni pigo kubwa kwa tasnia ya filamu kutokana na uzoefu, maarifa na moyo wake wa kuwalea vijana.

Muigizaji JB ambaye amefanya kazi hivi karibuni na marehemu kwenye tamthilia inayoendelea kuoneshwa YouTube, amesema kuwa marehemu ameacha pengo lisilofichika mioyoni mwa wengi.

“Nitamkumbuka kwa mambo mengi. Tumefanya kazi pamoja katika filamu mbalimbali na alikuwa mtu aliyependa kuona wasanii vijana wanakua na kufanikiwa,” amesema.

Naye Steve Nyerere amesema Mzee Onyango ameacha somo la kujituma na kuipenda sanaa bila kujali umri.

“Alikuwa mtu wa kazi. Hata alipokuwa amezeeka bado alikuwa tayari kushiriki shughuli za sanaa. Hilo ni funzo kubwa kwa kizazi cha sasa cha wasanii,” amesema.

Marehemu ameacha watoto 10, wajukuu 12 na vitukuu 12, huku urithi wake wa sanaa ukiendelea kuishi katika vizazi vya wasanii na mashabiki walioguswa na kazi zake.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi