Na Mwandishi wetu
Bagamoyo. Wanafunzi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA) wanatarajiwa kushiriki mjadala maalum wa Music & Film Business Session utakaowakutanisha na wataalamu wa muziki na filamu kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu biashara na fursa zilizopo katika uchumi wa ubunifu.
Mjadala huo utafanyika Juni 19, 2026 katika ukumbi wa TASUBA na utajadili masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kujenga taaluma endelevu, kutumia mitandao ya kitaaluma, kutambua fursa za biashara pamoja na kuelewa nafasi ya uchumi wa ubunifu katika ukuaji wa sekta ya sanaa.
Miongoni mwa wazungumzaji watakaoshiriki ni mtaalamu wa biashara ya muziki na meneja wa msanii Alikiba, Benjamin Otwal, pamoja na wadau wa filamu Eliya Mjatta, ambaye ni Rais Mstaafu wa Shirikisho la Filamu Tanzania, na Conrad Kashasha, mtangazaji wa televisheni na muigizaji.
Mratibu wa tukio hilo, Stellabeatrice Benedict, ambaye pia ni mhitimu wa TASUBA katika fani ya Uzalishaji wa Filamu na Televisheni, amesema lengo la mjadala huo ni kuwasaidia vijana kuelewa kuwa mafanikio katika tasnia za ubunifu hayategemei kipaji pekee bali yanahitaji pia uelewa wa biashara, mahusiano ya kitaaluma na uwezo wa kutumia fursa zilizopo.
“Tunaamini vijana wengi wenye vipaji wanahitaji pia maarifa ya biashara na mbinu za kujenga taaluma zao kwa muda mrefu. Kupitia mjadala huu tunatarajia kuwapa mwanga na kuwaunganisha na wataalamu waliopo kwenye tasnia,” amesema Stellabeatrice.
Amesema tukio hilo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mazungumzo kuhusu uchumi wa ubunifu na kuwapa vijana maarifa yatakayowasaidia kujenga ajira na biashara zenye tija katika sekta za muziki, filamu na sanaa kwa ujumla.
