Na Charles Mkoka
KIGAMBONI – Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kigamboni, Lilian Wasira, kupitia kampuni yake ya burudani ya Wasira Entertainment kwa kushirikiana na Chama cha Waigizaji Wilaya ya Kigamboni (TDFAA), wameandaa usaili mkubwa (audition) wa kutafuta vipaji vya uigizaji kwa ajili ya utengenezaji wa filamu fupi yenye ujumbe wa kupinga unyanyasaji wa kijinsia.
Kwa mujibu wa waandaaji, mradi huo unalenga kutoa fursa kwa vipaji vipya kujitokeza na kushiriki katika kazi ya sanaa itakayobeba ujumbe wa elimu kwa jamii kuhusu athari za unyanyasaji wa kijinsia na umuhimu wa kulinda haki za wanawake na watoto.
Filamu hiyo fupi inatarajiwa kutengenezwa kwa viwango vya juu vya kitaalamu, huku ikikusudia kufikisha ujumbe kwa hadhira pana kupitia simulizi litakalogusa changamoto zinazolikabili jamii katika masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Mbali na kutumika kama jukwaa la kukuza vipaji vya waigizaji wa Kigamboni na maeneo mengine, mradi huo pia unatarajiwa kuwa sehemu ya kampeni ya uhamasishaji wa jamii kuhusu mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Waandaaji wameeleza kuwa baada ya kukamilika kwa uzalishaji, filamu hiyo itazinduliwa katika hafla kubwa ya kisasa itakayofanyika Kigamboni.
Mgeni rasmi anayetarajiwa kuhudhuria uzinduzi huo ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, pamoja na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Kigamboni.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya jitihada za kutumia sanaa kama chombo cha kuelimisha, kuhamasisha mabadiliko ya kijamii na kuibua vipaji vipya vinavyoweza kuchangia maendeleo ya tasnia ya filamu nchini.

