Jimmy Mafufu azindua ofisi mpya za kutengeneza filamu Dar es Salaam

 Na Mwandishi wetu 

Mtayarishaji wa filamu na muundaji wa tamthilia ya Panguso, Jimmy Mafufu, amezindua rasmi ofisi mpya za kampuni yake pamoja na vifaa vya kisasa vya uzalishaji wa maudhui katika hafla iliyofanyika Kinondoni, Dar es Salaam.

Uzinduzi huo ulifanywa na Katibu Mtendaji wa Tanzania Film Board, Gervas Kasiga ambaye alimpongeza Mafufu kwa uwekezaji alioufanya katika kukuza uwezo wa uzalishaji wa filamu na maudhui ya ubunifu nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Kasiga alisema uwekezaji wa miundombinu na teknolojia za kisasa ni moja ya nguzo muhimu za kukuza ushindani wa tasnia ya filamu Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Askofu Mwaisabila pamoja na mke wake Ester Mwaisabila, ambao ni babu na bibi wa Jimmy Mafufu. Mama yake Jimmy, Debora Mwaisabila, naye alishiriki katika tukio hilo pamoja na viongozi na wadau mbalimbali wa tasnia ya filamu.

Miongoni mwa wageni waliohudhuria ni Chick Mchoma pamoja na watendaji wa kampuni hiyo.

Kwa upande wake, Jimmy Mafufu alitoa shukrani kwa viongozi, familia, marafiki na wadau wa tasnia ya filamu waliojitokeza kushuhudia hatua hiyo mpya katika safari yake ya ubunifu.

Uzinduzi wa ofisi hizo unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za Mafufu kuimarisha uzalishaji wa maudhui ya filamu na televisheni, huku akiwa miongoni mwa watayarishaji wanaoendelea kujijengea jina kupitia kazi mbalimbali ikiwemo Panguso, moja ya tamthilia zilizowahi kuvutia watazamaji wengi nchini.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi