Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Wasanii wa filamu na sanaa nchini wameahidi kutumia umaarufu wao kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, wakisema elimu hiyo inapaswa kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan wanawake na wakazi wa vijijini.
Akizungumza baada ya kushiriki semina kuhusu nishati safi, ilioandaliwa na TZLPGA, msanii wa filamu Rosemary Gaspard Kua alisema matumizi ya gesi yameleta mabadiliko makubwa katika maisha yake ya kila siku.
"Ningependa kuwaona wanawake wengi wakiacha matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye nishati safi. Gesi inaokoa muda, inapunguza usumbufu na inarahisisha maisha," alisema.
Rosemary alisema yeye pamoja na wasanii wenzake wamejipanga kuendelea kutoa elimu katika maeneo mbalimbali ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu faida za nishati safi.
Kwa upande wake, msanii Yahya Jeneto alisema elimu waliyoipata imewapa jukumu la kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii.
"Sasa ni wakati wa kuifikisha elimu hii vijijini. Tunataka kuona wananchi wengi zaidi wakifahamu faida za kutumia gesi badala ya kuni na mkaa," alisema.
Aliongeza kuwa matumizi ya gesi yana faida kwa mazingira, afya na uchumi wa familia, huku akiiomba Serikali kuendelea kuweka mazingira yatakayosaidia wananchi wengi kumudu gharama za nishati safi.
Naye msanii mkongwe Abdala Saidi Suleman maarufu kwa majina mbalimbali ya kisanii ikiwemo Mzee Kolezo, alisema changamoto kubwa bado ipo kwa wananchi wa vijijini ambao wanaendelea kutegemea kuni kwa sababu ya ukosefu wa elimu na gharama za nishati mbadala.
"Tukiwafikia watu wa vijijini na kuwapa elimu sahihi, tutalinda mazingira, tutalinda afya zao na tutalinda vizazi vijavyo," alisema.
Alisema wasanii hawatabaki kwenye majukwaa pekee bali watatumia maigizo, vichekesho na mikutano ya kijamii kueneza ujumbe wa matumizi ya nishati safi.
"Tumepewa moto wa mabadiliko. Kazi yetu sasa ni kuupeleka kwa wengine ili nao wawe sehemu ya safari ya nishati safi Tanzania," alisema.
Wadau wa nishati wanaamini ushiriki wa wasanii unaweza kuongeza kasi ya uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi na kusaidia kufikia malengo ya taifa ya kupunguza matumizi ya nishati chafu za kupikia.


