|
“Mwenyekiti wa Taasisi ya Wazee Waigizaji Tanzania akishiriki zoezi la upimaji wa macho.” |
Na Charles Mkoka
Dar es Salaam, 9 Septemba 2025 – Taasisi ya Wazee Waigizaji Tanzania kwa kushirikiana na Manispaa ya Ubungo kupitia Ofisi ya Mganga Mkuu wa Manispaa (DMO), na Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia Kitengo cha Upimaji Afya, imeandaa zoezi la bure la upimaji wa afya kwa wakazi wa jiji.
Zoezi hilo litafanyika tarehe 16 Septemba 2025, kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni, katika viwanja vya Kanisa Katoliki Mburahati.
Kwa mujibu wa waandaaji, huduma zitakazotolewa ni pamoja na upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu, kisukari, na matatizo ya moyo.
Aidha, kutatolewa pia huduma ya reflexology, ambayo ni tiba inayohusisha uchua wa mishipa katika nyayo za miguu, itakayotolewa na kituo cha tiba kilichopo eneo la kanisa.
Huduma zote zitakuwa bure kwa wananchi.
Hii ni mara ya pili kwa Taasisi hiyo kufanya upimaji wa afya tangu kuanzishwa kwake. Zoezi la kwanza lilihusisha upimaji wa macho na lilidhaminiwa na Rais wa Shirikisho, Bw. Rajabu Amiry, pamoja na Makamu wake, Bi. Godliver Godian.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Taasisi hiyo, Bi. Heriety Chumira, upimaji huu wa sasa unafanyika baada ya Taasisi kuomba nafasi hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, ambaye aliratibu mazungumzo na Mganga Mkuu wa Manispaa kuratibu utekelezaji wake.
“Lengo letu ni kusaidia jamii kwa kutoa huduma muhimu za afya bure, ili kuongeza uelewa na kuboresha maisha ya wananchi,” alisema Chumira.