Na Charles Mkoka
Dar es Salaam. Tamasha la Sauti Zetu Film Festival limeendelea kuibua gumzo katika tasnia ya filamu Afrika Mashariki, likiwa jukwaa la kipekee linalounganisha watengeneza filamu, jamii na wadau wa sanaa.
Muandaaji wa tamasha hilo, Sheilla Kipuyo, amesema kuwa kwa misimu mitatu mfululizo tangu 2023, Sauti Zetu Film Festival (SZFF) limekuwa daraja kati ya wasanii na jamii.
“Tamasha hili limekuwa na mchango mkubwa, si tu kwa kuonesha filamu, bali pia kwa kutoa mafunzo kuhusu ubora wa utengenezaji na namna ya kuuza kazi. Tuna workshop zinazomalizika kwa screening ya filamu tunazopokea, jambo linalowajengea ujasiri watengeneza filamu wetu,” alisisitiza Bi. Sheilla.
Kwa miaka miwili iliyopita, tamasha limefanyika Little Theatre kwa siku mbili jijini Dar es Salaam na Mkuranga mkoa wa Pwani kwa siku ya tatu, likiwakutanisha vikundi vya filamu vya ndani na nje ya nchi.
Kwa mwaka huu wa 2025, tamasha limepanua wigo hadi Arusha, hatua inayochukuliwa kama fursa ya ukuaji na ushirikishwaji wa jamii moja kwa moja mitaani.
Majaji wa tamasha wanatoka mataifa mbalimbali ikiwemo Kenya, Uganda, Tanzania na Afrika Kusini, kuhakikisha kiwango cha kimataifa kinapimwa bila kupoteza asili ya Kiafrika.
Filamu ambazo hazikidhi maadili ya Kitanzania huchujwa, huku zile zinazopitishwa zikioneshwa kwenye maonesho rasmi ya tamasha.
Bi. Sheila ameeleza kuwa tamasha pia lina ushirikiano wa karibu na Bodi ya Filamu Tanzania, kuhakikisha kazi zote zilizopokelewa zinakaguliwa kwa mujibu wa taratibu.
“Utaratibu huu umekuwa na matokeo chanya ya kukuza na kuendeleza sekta yetu ya filamu nchini,” aliongeza
Kwa mwaka huu, tamasha limekuwa na mwamko mpya wa kijinsia, ambapo zaidi ya filamu tatu zimezalishwa na wanawake kutoka Afrika Mashariki.
“Hii ni hatua ya kimaendeleo yenye maana kubwa kwa wanawake katika tasnia ya filamu, na tunajivunia kuona sauti zao zikisika kupitia kazi zao,” alifafanua Bi. Sheila.
Mbali na maonesho jijini Dar es Salaam na Arusha, Sauti Zetu pia limefika Mkuranga, ambako jamii iliburudishwa na maonesho ya filamu tatu za Kitanzania, maigizo ya jukwaani na burudani kutoka kwa kikundi cha muziki cha Jagwa.
Ingawa mwaka huu hakukuwa na usiku wa tuzo, waandaaji wameeleza kuwa lengo kubwa limekuwa ushirikishwaji wa jamii zaidi na kuongeza mtandao wa filamu za kanda nzima. Filamu kutoka Rwanda na Burundi zimeongeza upekee wa tamasha la mwaka huu.
Kwa mtazamo wa mbele, Sauti Zetu Film Festival inalenga kupanua wigo hadi mikoa mingi zaidi ya Tanzania, ikibaki kuwa nguzo muhimu ya kukuza tasnia ya filamu barani Afrika.

