FEKI: Web Series Inayojengwa Kwa Jasho, Uvumilivu na Maono ya Muda Mrefu


Na Mwandishi Wetu

Tamthilia mpya ya mtandaoni FEKI, inayozalishwa na 2Ghaa Films, imeingia kambini kwa muda wa mwezi mmoja kwa ajili ya kukamilisha msimu wa kwanza wa web series hiyo inayorushwa kupitia YouTube.

Akizungumza na Sauti za Filamu, Mkurugenzi wa 2Ghaa Films, Atuganile Abraham Mwakalobo, amesema msimu wa kwanza wa FEKI unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Februari, baada ya mchakato wa uzalishaji uliofanywa kwa awamu.

“Tulianza kwa kushuti episode kumi, tukapumzika kidogo, halafu tukaendelea kushuti episode chache chache. Zoezi limekuwa endelevu, lakini kambi hii itatupa zaidi ya episode 50 zitakazokamilisha msimu mzima,” amesema Atuganile.

Kwa mujibu wake, awamu za mwanzo za uzalishaji pia zilikuwa kama sehemu ya mchujo wa kimyakimya wa vipaji, si kwa waigizaji pekee bali pia kwa crew nzima ya tamthilia hiyo.

“Vijana walikuwa wanashuti kama kazi ya kawaida, lakini kwangu nilikuwa naangalia uwezo wao. Ilikuwa ni majaribio ya kutambua talents kuanzia wasanii, waandishi wa miswada, wapiga picha, taa, mavazi hadi wasimamizi wa kazi,” amesema.

Atuganile amesema ndoto yake kubwa ni kuanzisha academy ya filamu itakayokuza na kuendeleza tasnia nchini Tanzania, akibainisha kuwa tayari amewekeza binafsi kwa zaidi ya miaka sita bila kutegemea ufadhili wa nje.

“Ninagharamia kila kitu mwenyewe. Ni mwaka wa sita sasa, na matokeo yamekuwa ya kuridhisha. Nime-train directors, lighting crew, costume designers, script writers, supervisors, cast managers—zaidi ya watu kumi, na natamani waendelee kukua,” amesema.

Mwakalobo, ambaye amewahi kufanya kazi na wasanii wakubwa akiwemo Monalisa, Natasha na Shija katika tamthilia ya Maza Hausi tangu mwaka 2008, amesema kwa sasa ameamua kuwekeza kikamilifu kwenye filamu, huku akiendeleza ujuzi wake wa uandishi wa miswada na uigizaji.

Amesisitiza kuwa hana haraka ya kukimbilia majukwaa makubwa ya kibiashara kama Azam au DStv bila kupata kile anachokiamini katika tasnia.

“Sifikirii kukimbilia pesa ya haraka. Unaweza kulipwa milioni 100 au 200 kwa tamthilia moja, lakini baada ya hapo maisha yatakuwaje? Mimi nimewekeza kwenye nguvukazi,” amesema.

Kwa mujibu wake, changamoto kubwa katika tasnia ya filamu Tanzania ni thamani ndogo ya msanii, hali inayochangiwa na utamaduni wa kufanya kazi bila mifumo rasmi.

“Wasanii wamezoea kuitana, kushuti scene mbili tatu na kulipana elfu tano. Hii inadumaza tasnia. Inaonekana kama wanapata, lakini mwisho wa siku hakuna maendeleo,” amesema.

Ameongeza kuwa uwepo wa agencies za kitaaluma unaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kukuza tasnia kwa kuimarisha professionalism, kama ilivyo katika nchi nyingine ambako hata content influencers wana agencies zao.

Licha ya 2Ghaa Films kutokuwa active sana mitandaoni kwa muda mrefu, Atuganile amesema walikuwa wanawekeza zaidi kwenye elimu, mafunzo na uboreshaji wa ndani. Matokeo yake, akaunti yao ya YouTube imekua kutoka subscribers 2,000 hadi zaidi ya 33,000.

2Ghaa Films ina makao makuu Kibaha, Dar es Salaam, na FEKI imeanza kupata mwitikio mkubwa kutoka kwa watazamaji.

“Nimepokea testimonies nyingi kutoka sehemu mbalimbali nchini. Watu wanasema wameguswa na matukio wanayoyaona, kwa sababu yanahusiana na maisha halisi ya kazini. Nawashukuru wote wanaoendelea ku-support kazi zetu,” amesema.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi