Tuzo za Filamu Tanzania zapata hadhi ya kimataifa, Filamu 2,360 zapokelewa


 Na Mwandishi wetu

Mchakato wa Tuzo za Filamu Tanzania (TAFFA) umeendelea kuchukua sura mpya huku tasnia ya filamu nchini ikiendelea kujipambanua kimataifa. 

Tuzo hizo, ambazo sasa zimeingia msimu wa nne, zinatarajiwa kutolewa rasmi tarehe 14 Februari katika ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutangaza waigizaji na watayarishaji walioteuliwa kuwania tuzo hizo, Mkurugenzi wa Studio 19, Bw. Brian M. Paul, amesema mchakato wa tuzo umeingia katika hatua ya tatu, ambayo ni hatua ya kutambua na kutunuku ubora.

“Baada ya tamasha la filamu mwezi Agosti, tuliendelea kupokea filamu kutoka Tanzania, Afrika Mashariki na sehemu nyingine za dunia. Dirisha la kupokea filamu lilifungwa mwezi Septemba, ndipo jopo la majaji na wataalamu wa kifundi lilipokaa chini kuzihakiki kwa umakini mkubwa,” amesema Brian.

Amefafanua kuwa kazi ya majaji haikuwa rahisi, ikihusisha muda mwingi na uchambuzi wa kina ili kuhakikisha filamu zinazoteuliwa zinaakisi ubora wa hali ya juu wa tasnia ya filamu ya Tanzania, akiwapongeza kwa weledi na kujitoa kwao bila kuchoka.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Bw. Rajabu Amir, amesema kuwa pamoja na mafanikio yaliyofikiwa, bado kuna haja ya kuongeza motisha kwa washindi wa tuzo hizo.

“Nimeomba serikali iangalie eneo hili kwa jicho pana zaidi. Tuzo isiishie kuwa sanamu na pongezi tu. Mtu akipokea tuzo, asiondoke akiwa na heshima pekee, bali pia akiwa na kitu chenye thamani kitakachomsaidia kubadilisha maisha na kuendelea na kazi zake,” amesema Amir.

Ameongeza kuwa mazungumzo na wadau wa maendeleo yanaendelea, huku akibainisha kuwa bado hawajafikia makubaliano ya mwisho, lakini matumaini ni makubwa kutokana na muda uliobaki kabla ya tuzo kufanyika.

“Tuna mwezi mzima wa kukaa mezani na wadau. Lengo ni kuhakikisha anayeshinda tuzo anaondoka akiwa amepata kitu kinachoendana na thamani ya kazi yake,” ameongeza.

Aidha, Amir amesisitiza kuwa kushinda au kutoshinda hakupaswi kuvunja moyo wa wanatasnia, akibainisha kuwa ushindani ni sehemu ya ukuaji wa tasnia.

“Hatuwezi kuwa na gari linalobeba kila mtu. Tunachagua wachache kwa wakati husika. Asiyepata tuzo aongeze bidii, si kujiona ameshindwa,” amesema.


Naye Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, amesema kuwa Tuzo za Filamu Tanzania 2025 zimevutia ushiriki mkubwa wa filamu kutoka mataifa mbalimbali, jambo linalozipa tuzo hizo hadhi ya kimataifa.

Dkt. Kasiga amesema kuwa jumla ya filamu 2,360 zilipokelewa, kati ya hizo filamu 239 zinatoka Tanzania, huku filamu 2,121 zikitoka mataifa mengine duniani.

“Tunawapongeza wanatasnia wote walioteuliwa kuwania tuzo hizi katika vipengele 26 vilivyotangazwa. Hatua ya kuteuliwa yenyewe ni ushindi mkubwa, kwa kuwa inaashiria kutambuliwa miongoni mwa wengi wanaofanya kazi za filamu,” amesema Dkt. Kasiga.

Dkt. Kasiga pia amewapongeza na kuwashukuru Studio 19, waandaaji wa Tuzo za Filamu Tanzania, kwa kazi kubwa na juhudi walizozionyesha katika kuandaa tuzo hizo kwa misimu minne mfululizo.

Aidha, ametoa shukrani za pekee kwa Azam Media Limited kwa kuendelea kudhamini tuzo hizo tangu mwaka 2021, akieleza kuwa mchango wao umekuwa muhimu katika kuhakikisha tuzo zinaendelea kufanyika kwa viwango vya juu.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Filamu, Bw. Emmanuel Ndumukwa, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi kutoka Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Asha Ngatila, Mkuu wa Chaneli ya Sinema Zetu ya Azam TV, Bi. Sophia Mgaza, pamoja na viongozi wa Studio 19 akiwemo Bw. Sama Jahanpour na Bw. Brian M. Paul.

Tuzo za Filamu Tanzania 2025/2026 zinatarajiwa kutolewa rasmi tarehe 14 Februari 2026 katika ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam, zikitarajiwa kuwakutanisha wadau wa filamu kutoka ndani na nje ya nchi

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi