Na Mwandishi wetu
Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) zimeazimia kuimarisha na kuendeleza ushirikiano wao kwa lengo la kuzitangaza fursa za utalii zilizopo nchini kupitia filamu na michezo ya kuigiza.
Hatua hiyo imebainishwa katika kikao kilichofanyika leo Alhamisi, tarehe 8 Januari 2026, katika ofisi za Bodi ya Utalii Tanzania jijini Dar es Salaam,
katika kikao hicho, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, alikutana na Mkurugenzi wa Idara ya Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania, Ndg. Ernest Mwamwaja, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Ndg. Ephraim Balozi Mafuru.
Shabaha kuu ya kikao hicho ilikuwa kujadili namna bora ya kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya taasisi hizo mbili katika kutumia filamu kama nyenzo muhimu ya kuitangaza Tanzania kama kivutio cha utalii, ndani na nje ya nchi.
Dkt. Kasiga amesema kuwa filamu na michezo ya kuigiza vina mchango mkubwa katika kuonesha utajiri wa vivutio vya utalii vilivyopo nchini, ikiwemo mandhari ya asili, utamaduni na urithi wa Taifa.
Amebainisha kuwa ushirikiano kati ya Bodi ya Filamu na Bodi ya Utalii ni hatua muhimu katika kuhakikisha tasnia ya filamu inanufaika, sambamba na kuongezeka kwa mwonekano wa Tanzania kimataifa kupitia maudhui ya ubunifu.
Dkt. Kasiga aliambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Filamu, Ndg. Emmanuel Ndumukwa, pamoja na viongozi wa Mradi wa Guardians of the Peak, Bw. Ram Ally na Bi. Shuyan Wangu (Elizabeth Mrembo), ambao ni wadau wakubwa katika sekta za filamu na utalii nchini.
Mradi wa Guardians of the Peak, unaoingia msimu wake wa pili, unaandaa makala ya filamu inayolenga kuhamasisha shughuli za utalii katika Mlima Kilimanjaro, kuhimiza matumizi ya nishati safi pamoja na kuongeza uelewa wa athari za mabadiliko ya tabia ya nchi katika jamii.
Ushirikiano kati ya Bodi ya Filamu Tanzania, Bodi ya Utalii Tanzania na Mradi wa Guardians of the Peak umetajwa kuwa fursa mpya ya kuutangaza utalii wa Mlima Kilimanjaro kupitia filamu, ndani na nje ya Tanzania.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutumia sanaa na filamu kama nyenzo ya kimkakati ya kuitangaza nchi na vivutio vyake vya kipekee.