Na Mwandishi wetu
Watengenezaji wa filamu kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali duniani wamepata fursa mpya ya kupeleka kazi zao katika jukwaa la kimataifa baada ya Tamasha la Kimataifa la Filamu la Mumba, linalojulikana kama Mumba International Film Festival (MIFF), kutangaza rasmi kufunguliwa kwa dirisha la kuwasilisha filamu kwa toleo lake la saba litakalofanyika mwaka 2026 nchini India.
Kwa mujibu wa waandaaji wa tamasha hilo, dirisha la kuwasilisha filamu limefunguliwa tangu tarehe 1 Januari 2026 hadi 31 Machi 2026 na lipo wazi kwa watengenezaji wa filamu kutoka pande zote za dunia, wakiwemo wabunifu kutoka Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika kuanzia Tarehe 25 hadi 30 Julai 2026 katika ukumbi wa National Film Archive of India uliopo Pune, katika Jimbo la Maharashtra, moja ya maeneo muhimu ya kihistoria kwa tasnia ya filamu nchini India.
MIFF ni jukwaa linalolenga kukuza ubunifu wa filamu, kuunganisha watengenezaji wa filamu kimataifa na kutoa nafasi kwa hadithi zenye mitazamo tofauti kuonekana katika majukwaa ya dunia.
Kwa toleo la 2026, tamasha linapokea filamu ndefu (dakika 60 - 140), filamu fupi (dakika 1 - 60), makala, filamu za uhuishaji, filamu za wanafunzi pamoja na filamu za sekunde 90 (skits/reels ambazo zinatakiwa kuwa wima/horizontal).
vinara kuzawadiwa kitita cha Tshs. 1,419,679 kwa mshindi wa filamu ndefu, Tshs. 583,575 kwa filamu fupi, Tshs. 277,885 kwa skits/reels, huku kukiwa na zawadi pia za pesa taslimu kwa washindi wa pili na wa tatu. kwa upande wa Animation na Makala (Documentaries) watapokea kiasi cha Tshs. 138,942 kwa vinara pekee
Waandaaji wamesisitiza kuwa filamu zote zisizo za lugha ya Kiingereza zinapaswa kuwa na manukuu ya Kiingereza (English subtitles) ili kuwezesha tathmini ya kimataifa na mawasiliano kwa hadhira pana.
Uwasilishaji wa filamu unafanywa mtandaoni pekee kupitia jukwaa la FilmFreeway na Google Forms vikitumika, huku viunganishi vya kutazama filamu kupitia Vimeo, YouTube au Google Drive vikikubalika.
Kuna gharama ya kuwasilisha filamu ambayo hairudishwi, (inaanzia Tshs. 41,000 kwa filamu fupi hadi tshs 276,822 kwa filamu ndefu, inategemea na dakika za filamu yako) na taarifa zote zinapatikana kupitia tovuti rasmi ya tamasha hilo pamoja na kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Filamu zitakazochaguliwa zitapata fursa ya kushindania tuzo na vyeti, kuoneshwa mbele ya wadau wa kimataifa wa tasnia ya filamu, na kufungua milango ya kushiriki katika majukwaa mengine ya kimataifa.
Endapo filamu itachaguliwa, mtengenezaji anaweza kualikwa kuhudhuria tamasha hilo nchini India, ingawa gharama za usafiri na malazi kwa kawaida hujigharamia binafsi.
Licha ya hilo, MIFF inaelezwa kuwa ni moja ya majukwaa yanayotoa mwonekano mpana kwa filamu huru na sauti mpya katika tasnia ya filamu duniani.
Tamasha la Kimataifa la Filamu la Mumba linaonekana kuwa fursa muhimu kwa watengenezaji wa filamu wa Tanzania kupeleka simulizi zao katika jukwaa la dunia na kuimarisha uwepo wa hadithi za Kiafrika katika tasnia ya filamu ya kimataifa.
Taarifa zaidi zinapatikana kupitia tovuti rasmi ya tamasha www.mumbafilmfestival.com pamoja na kiunganishi cha uwasilishaji kupitia FilmFreeway na ukurasa wa Instagram wa tamasha hilo
Haya na mengine mengi yanapatikana pia kwenye kurasa na Tovuti ya Bodi ya filamu nchini