Wasanii kukutana Pande kwa Tamasha la Sanaa na Utalii


Na Mwandishi Wetu

Vyama vya Waigizaji Tanzania (TDFAA) vilivyopo mkoa wa Dar es Salaam, (Ubungo, ilala, kigamboni kinondoni na temeke) kwa kushirikiana na chama cha waigizaji wa Mkoa wa Dar es salaam, kimetangaza kuandaa tamasha la sanaa na utalii lijulikanalo kama Pande Arts & Utalii Festival, litakalofanyika katika Pori la Akiba la Pande tarehe 10 Februari 2026.

Kwa mujibu wa waandaaji, wasanii watasafiri kwa pamoja kwenda Pande tarehe 10 Februari na kurejea Dar es Salaam tarehe 11 Februari 2026, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mshikamano wa wasanii pamoja na kuitangaza sanaa kama chombo cha kukuza utalii wa ndani.

Tamasha hilo liko wazi kwa wasanii wote walio wanachama hai wa TDFAA kutoka wilaya zote za Dar es Salaam, ambapo ushiriki wao utakuwa bure kabisa, huku gharama zote zikiwemo usafiri, chakula na vinywaji zikisimamiwa na chama.

Kwa wasanii wasio wanachama hai wa TDFAA, pamoja na ndugu, marafiki au wageni wanaotaka kushiriki, waandaaji wamesema kuwa gharama ya ushiriki ni Shilingi 20,000, kiasi kinachojumuisha usafiri, chakula na vinywaji.

Waandaaji wamesema Pande Arts & Utalii Festival inalenga kuunganisha sanaa na utalii, kuimarisha mahusiano kati ya wasanii na kutoa jukwaa la kuhamasisha utalii wa ndani kupitia ubunifu wa wasanii wa Tanzania.

Tamasha hilo linatajwa kuwa fursa muhimu kwa wasanii kusherehekea sanaa, kubadilishana uzoefu na kuifahamu Pande kama moja ya vivutio vya utalii vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi