Guardians of the Peak msimu wa pili kuangazia uhifadhi wa Mlima Kilimanjaro


Na Mwandishi wetu

Kuelekea uzinduzi wa utayarishaji wa msimu wa pili wa makala ya Guardians of the Peak, Bodi ya Filamu Tanzania imeeleza dhamira ya serikali kuendelea kuunga mkono miradi ya filamu inayolenga uhifadhi wa mazingira na kuitangaza Tanzania katika jukwaa la kimataifa.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Filamu Ndugu Emmanuel Ndumukwa amesema kuwa mradi wa Guardians of the Peak umejikita katika kulinda Mlima Kilimanjaro, urithi wa taifa na nembo ya Tanzania inayotambulika duniani kote.

Ndumukwa aliyasema hayo leo, Januari 14, 2026, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya King Jada, Kinondoni–Morocco, jijini Dar es Salaam.

Amesema kupitia Guardians of the Peak – Msimu wa Pili, dunia itapata fursa ya kuona kwa kina changamoto za kimazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi, umuhimu wa uhifadhi wa maliasili, pamoja na jitihada za Tanzania katika kulinda urithi wake wa asili na kuendeleza utalii endelevu.

“Mradi huu unaonesha namna filamu inavyoweza kuwa chombo muhimu cha kuelimisha jamii, kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na wakati huo huo kuitangaza Tanzania katika ramani ya kimataifa,” amesema Ndumukwa.

Aidha, amewahakikishia waandaji wa mradi huo kuwa Serikali kupitia Bodi ya Filamu Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano na msaada kwa waandaaji hao na miradi mingine inayotumia filamu kama nyenzo ya kuleta mabadiliko chanya ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.

Katika hatua nyingine, Ndumukwa ametoa wito kwa wadau wa filamu na michezo ya kuigiza, taasisi za serikali, sekta binafsi pamoja na vyombo vya habari kuendelea kuunga mkono miradi ya aina hii kwa maslahi mapana ya taifa na maendeleo ya sekta ya filamu nchini.

Kwa mujibu wa waandaji, utayarishaji wa makala hiyo, Msimu wa Pili unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 20 Januari, 2026.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi