Msimu wa pili wa 'Guardians of the Peak' kuzinduliwa

Na Mwandishi wetu 

Dar es Salaam. Mradi wa filamu unaolenga kutangaza uhifadhi wa mazingira, utalii endelevu na ushirikiano wa kimataifa, ‘Guardians of the Peak’, unazindua rasmi trela ya msimu wake wa pili leo jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi huo unawakutanisha wadau wa utalii, mazingira, sekta ya filamu, wawekezaji pamoja na viongozi kutoka Tanzania na China.

Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, huku Mkurugenzi wa Kituo cha Utamaduni cha China nchini Tanzania, Xing Lijun, akihudhuria kama mgeni maalum.

Waandaaji wanasema msimu mpya utaendelea kutumia nguvu ya filamu kuhamasisha uhifadhi wa Mlima Kilimanjaro, matumizi ya nishati safi na maendeleo ya utalii wenye tija kwa jamii.

Mradi huo pia unalenga kuwapa vijana fursa kupitia sanaa, elimu na ushirikiano wa kimataifa.

Trela hiyo ni hatua muhimu kuelekea uzinduzi rasmi wa ‘Guardians of the Peak’ Season II, unaotarajiwa kufanyika Julai 18 mwaka huu.

Kupitia kaulimbiu ya “Protecting the Peak, Empowering the Future”, waandaaji wanaamini filamu inaweza kuwa daraja la kuunganisha uhifadhi wa mazingira, maendeleo ya utalii na fursa za kiuchumi kwa kizazi kijacho.

Kwa Tanzania, mradi huo unaendelea kuitumia Kilimanjaro kama nembo ya kutangaza urithi wa asili wa nchi na kuvutia watazamaji wa kimataifa.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi