Kikundi kipya cha wasanii wa filamu nchini kinachoitwa Mkono wa Faraja kimeanzishwa kwa lengo la kuimarisha mshikamano na kutoa msaada kwa waigizaji wanapokumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo maradhi, misiba na matatizo mengine ya kijamii.
Akizungumza katika mahojiano na Sauti za Filamu, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Ibrahim Msuka, amesema wazo la kuanzisha Mkono wa Faraja limekuja baada ya kuona wasanii wengi wakipitia nyakati ngumu bila kuwa na mfumo wa pamoja wa kusaidiana.
Msuka alisema kikundi hicho kilianzishwa rasmi Mei 31, 2026 na tayari kimeanza kuvutia wanachama kutoka maeneo mbalimbali nchini.
“Lengo letu kubwa ni kuhakikisha msanii anapopata tatizo hajisikii yuko peke yake. Tunataka kuwe na mfumo wa haraka wa kusaidiana wakati wa ugonjwa, msiba au changamoto nyingine,” alisema.
Kwa mujibu wa Msuka, kikundi hicho kinaongozwa na timu ya viongozi inayojumuisha Makamu Mwenyekiti Madam Sapenga, Katibu Frola Tarimo, Katibu Msaidizi Ali Njenje na Mweka Hazina Maria Mramavani maarufu kama Mamrishas, huku wajumbe wakitoka miongoni mwa waigizaji wenye uzoefu katika tasnia hiyo.
Mbali na kusaidiana wakati wa matatizo, Msuka alisema Mkono wa Faraja unalenga pia kuwa jukwaa la kuunganisha waigizaji, madirector, maproducer na wadau wengine wa sanaa ili kufungua fursa zaidi za ajira na miradi ya ubunifu.
Alieleza kuwa ndani ya kikundi hicho tayari kuna wataalamu kutoka maeneo tofauti ya tasnia ya filamu, jambo ambalo linaweza kusaidia kuzalisha miradi mipya ya tamthilia, filamu na kazi nyingine za sanaa.
“Tunao waigizaji, madirector na maproducer. Fursa yoyote ikitokea, inaweza kuwafikia wanachama wetu moja kwa moja. Hili si kundi la kusaidiana tu, bali pia la kutengeneza fursa za maendeleo,” alisema.
Msuka alisema hadi sasa kikundi kina wanachama wanaokaribia 300 na kinakaribisha waigizaji kutoka mikoa yote ya Tanzania, mradi mtu awe anatambulika ndani ya tasnia hiyo.
Alisisitiza kuwa Mkono wa Faraja haujaletwa kuchukua nafasi ya vyama vya wasanii vilivyopo wala taasisi za serikali zinazoratibu sekta hiyo, bali unakusudia kushirikiana nazo kwa maslahi mapana zaidi ya wasanii.
“Kikundi hiki ni nyongeza ya juhudi zilizopo. Tunaendelea kuheshimu taratibu za Bodi ya Filamu na vyama vya wasanii. Tunataka ushirikiano, si ushindani,” alisema.
Kwa sasa Mkono wa Faraja bado unaunaendelea na taratibu zingine za usajili, na baadae, uongozi umeeleza kuwa hatua za kujitambulisha kwa wadau wa sekta ya filamu na taasisi husika unaendelea kadri kikundi kinavyoendelea kukua.
Msuka ametoa wito kwa waigizaji nchini kujiunga na kikundi hicho ili kujenga umoja, kuimarisha ustawi wa wasanii na kuongeza fursa za maendeleo ndani ya tasnia ya filamu Tanzania.